Natangulia kuwasalimu wapenzi wanablog. Bila shaka wote hamjambo. Leo ningependa niongelee juu ya tunda linaloonekana kwenye picha hapo juu. Tunda hili linajulikana kwa jina la Avocado, kwa lugha ya wenzetu, na kwa lugha yetu ya kiswahili tumezoea kuita kwa jina la Parachichi. Tunda hili lina majina mengi lakini nimeona niwatajie hayo mawili maana ndiyo "common" kwa watu walio wengi. Mimi binafsi, tunda hili nimelijulia hapa Bongo Darisalama nilipokuja miaka ile kwa mara ya kwanza. Siku ya kwanza kuonja tunda hili, sikulipenda na kwa kusema ule ukweli nililitema, maana sikuona ladha yeyote ile. Wakati huo, wale waliozoea kula tunda hili walinicheka sana.
Leo hii nawaambia, nimekuwa mlaji mzuri sana wa tunda hili, si kwamba ni tamu sana kuliko chochote, bali kutokana na umuhimu wake ambao nitauelezea hapo baadaye. Kwa asili, tunda hili limekuwa likizalishwa katika nchi zilizopo katika ukanda wa tropiki, hasa kule Amerika ya Kati. Lakini baadaye, zao hilo limesambaa na kulimwa maeneo mbalimbali hapa duniani. Huko nchi za ulaya wanalima, kule asia nako pia, hapa afrika napo tunajaribu na hata hapa Tanzania tumewekeza katika kilimo cha zao hilo muhimu kwa afya zetu. Maeneo machache yanayozalisha zao hili hapa nchini ni kama vile, kule kwa akina Mangi, yaani mkoani Kilimanjaro na kule kwa akina uswege, yaani mkoani Mbeya.
Kwa nini tunda hili lina umuhimu wa pekee! Labda ni kwa sababu ya virutubisho vyake vingi, vyenye uwezo wa kukinga na kutibu maradhi mbalimbali mwilini. Hebu fikiria kisa hiki;
" Hapo zamani za kale, palitokea mwanafunzi mmoja katika nchi za mbali, ambaye alifanya majaribio kwa kula avocado kwa kipindi cha mwezi mzima ikiwa kama ni mlo wake pekee kwa kila siku. Kijana huyo aliishi kwenye nyumba ya kupanga, na mwenye nyumba alichukua uamuzi wa kumfukuza katika nyumba yake, akihofia kuwa huenda angemletea matatizo na haibu endapo angemfia kwa kudhoofu kwa njaa. Lakini cha kushangaza kijana yule aliendeleza msimamo wake wa kula avocado kama alivyokusudia ingawa hakujua faida zinazopatikana kutokana na ulaji wa tunda hilo. Yule mwanafunzi alikuwa na ufahamu kidogo sana, kuwa matumizi ya muda mrefu ya tunda hilo yanaamsha ashki na kumfanya mtu awe na hamu na uwezo wa kutenda tendo la ndoa.
Hivi leo imethibitika kuwa tunda la avocado lina vitamini E ambayo ni muhimu katika kuimarisha mfumo wa uzazi kwa jinsia zote. Ukweli huu haupingani na ufahamu mdogo aliokuwanao yule kijana mwanafunzi wa enzi zile.
Tunda la avocado lina vitu gani zaidi ambavyo ni muhimu kwa afya yako, yangu na ya yule ndugu au jamaa yako! Endelea kufuatilia toleo lijalo. Tafadhali usikose, mwambie na mwenzio.
2FLAG
No comments:
Post a Comment