Thursday, September 18, 2008

UPUNGUFU WA NGUVU ZA KIUME (SEXUAL IMPOTENCE)

Hongera kwa saumu kwa wale waliofunga, na wale wenzangu na mie habari za siku tele. Ndugu zangu msidhani kama niliingia mitini bali dharura za kimaisha zilinizonga. Leo naomba nizungumzie kuhusu suala nyeti la upungufu wa nguvu za kiume na namna ambavyo mtu mwenye tatizo kama hili anaweza kutumia ushauri wangu ili kurejesha heshima yake katika kufanya mambo ya kikubwa. Hapo awali inasemekana tatizo hili lilisababishwa na sababu za kisaikolojia pamoja na uzee au umri mkubwa ambapo viungo vya mwili vinakuwa vimechoka.
Kwa miaka ya hivi karibuni imebainika kuwa sababu zinazosababisha upungufu wa nguvu za kiume zimeongezeka na zifuatazo ni baadhi ya sababu hizo, nazo ni;
  • Kutokana na mabadiliko ya kisayansi na kukua kwa teknolojia wanaume wengi wamekuwa wakiishi maisha rahisi ya kutotumia miili yao kwa kufanya kazi zinazotumia nguvu na matokeo yake mwili unashindwa kujenga misuli imara katika viungo mbalimbali vya mwili.
  • Ulaji wa vyakula vilivyopitia viwandani na vyenye asili ya mafuta na protini nyingi ambapo vyakula hivyo vinakosa virutubisho muhimu kwa ajili ya kuimarisha viungo nyeti. Vyakula vyenye asili ya mafuta vinasababisha kuwepo kwa cholestral kwenye damu ambayo inapunguza au kuzuia mzunguko wa damu kwenye nyeti za mwanaume na hatimaye kushindwa kufanya kazi vizuri.
  • Matumizi ya mara kwa mara ya vileo/pombe, kahawa, uvutaji wa sigara nayo yanachangia upungufu wa nguvu za kiume.
  • Athari za magonjwa kama kisukari, arteri, magonjwa ya neva yanayosababishwa na ulaji wa vyakula vyenye protini nyingi na mafuta mengi.
  • Ukosefu wa madini na vitamini mbalimbali zinazopatikana kwa wingi kutoka kwenye matunda na mbogamboga.

Kutokana na kero ya tatizo la upungufu wa nguvu za kiume au uhanithi, watu wengi wamekuwa wakijaribu kutumia vidonge ili waweze kuongeza nguvu na kufurahia tendo la ndoa. Imebainika kuwa matumizi ya vidonge hivyo yana madhara kwa afya ya mtumiaji. Baadhi ya athari anazoweza kuzipata mtumiaji wa dawa hizo ni pamoja na kuharisha, kichefuchefu, kuumwa na kichwa, kupooza baadhi ya viungo, upofu, kutosikia, na hata kupoteza kabisa kwa nguvu za kiume. Hali hiyo imewafanya watu wengi siku hizi wageukie matumizi ya dawa za mimea asilia au vyakula asilia ambapo havina athari kwa mtumiaji.

Hivyo basi mtu mwenye tatizo la uhanithi au upungufu wa nguvu za kiume anapaswa kuzingatia yafuatayo:

  • Kutumia kwa wingi matunda ikiwa kama sehemu ya mlo wake kila wakati anapopata mlo kwa siku tano hadi saba za mwanzo. Mtumiaji anaweza kuwa na milo mitatu kwa siku ambapo pia matumizi ya juisi ya zabibu, machungwa, apple, peas, nanasi, parachichi na tikitiki maji yanahimizwa.
  • Matumizi ya vyakula vya nafaka pia yanafufua matumaini kwa mtu aliyepoteza uweza wa kufanya tendo la ndoa kuweza kusimama upya. Inashauriwa pia mtumiaji atumie asali, mtindi, kitunguu saumu, mbogamboga na matunda mara kwa mara. Wakati huo huo mgonjwa aepuke matumizi ya sigara, pombe au vileo, kahawa, na vyakula vilivyopitia viwandani na vyenye protini na mafuta mengi.
  • Mazoezi ya viungo au mwili ama kufanya kazi zinazotumia nguvu nako kunasaidia kuimarisha viungo vya mwili. Iwapo mgonjwa atafanya kazi ya kutumia nguvu au mazoezi ya viungo japo dakika 30 hadi 45 kila siku na kisha kula vyakula vilivyoelezewa hapo juu anaweza kuwa na uwezo wa kusimama mwenyewe pasipo kutumia msaada wa vidonge vya kuongeza nguvu.

Pamoja na hayo machache mada ijayo nitaendeleza kutaja baadhi ya vyakula, matunda na matumizi ya mbogamboga na kazi zake katika kufufua uwezo wa wanaume aliyepoteza nguvu za kiume.

KILA LA KHERI.

2Flag.

Wednesday, September 10, 2008

SAMAHANI WANABLOG

Napenda kuwaomba samahani wanablog kwasababu nimekuwa kimya kwa muda sasa. Sababu mojawapo ni kwamba kwa kipindi kisichopungua wiki moja iliyopita nilikuwa na dharura kiasi ambacho nimeshindwa kuwawekea matoleo mapya kwenye blog hii. Hata hivyo, hali hiyo inaweza kuendelea kwa siku kadhaa na pindi nitakapomaliza dharura zangu nitaendelea kuwapatia mada mbalimbali kama kawaida. Naomba uvumilivu wenu, tafadhali.

2flag.

Wednesday, September 3, 2008

JINSI YA KUPUNGUZA UNENE


Za leo! Mambo vipi! Hizi ndizo salamu za siku hizi hasa kwa vijana. Baada ya salamu hiyo naomba turudi kwenye mada ya leo ya jinsi ya kupunguza unene. Kwanza kabisa napenda kuwashauri watu wanene wasitumie vidonge/madawa ya kiwandani kwa lengo la kupunguza unene, kwani vidonge vina athari zake mwilini ukizingatia kuwa vina kemikali ambazo baadhi hubakia mwilini na kutengeneza sumu.


Watu wanashauriwa kutumia vitamini itokanayo na matunda na mbogamboga. Aidha, kwa mtu mnene kushinda na njaa siyo dawa au tiba sahihi ya kupunguza unene. Mtu anayetaka kupunguza unene/uzito ni vema akazingatia misingi ifuatayo:



  • Punguza kula chumvi nyingi maana chumvi inatunza maji mwilini ambayo pia yana mchango mkubwa katika kuongeza uzito wa mwili. Kwa kuacha kula chumvi nyingi maji yataweza kupungua mwilini kwa njia ya mkojo au jasho.


  • Ongeza kula vyakula vyenye madini ya potasium, calcium, na magnesium ambapo madini hayo yanapatikana kutoka kwenye mbogamboga mbichi na matunda au maziwa ya soya.


  • Kula vyakula vyenye wanga, punguza vyakula vyenye mafuta na protini.


  • Kunywa maji mengi kiasi cha lita 2 kwa siku na kwa kila siku.


  • Fanya mazoezi ya mwili/viungo japo kwa dakika 30 hadi 60 kila asubuhi. Kutembea ni mojawapo ya mazoezi.

Katika kuongezea vitu hivyo hapo juu, mlengwa anashauriwa pia kutumia;




  • Asali kijiko kimoja na kuchanganya nusu ndimu au limao kwenye maji yenye uvuguvugu kiasi cha glasi moja na kunywa mara kwa mara.


  • Matumizi ya cabbage pia yamethibitika kuwa na mchango mkubwa katika kupunguza unene kwani kemikali zilizomo ndani yake zinasaidia kuzuia wanga na sukari kubadilishwa kimfumo na kuwa mafuta ambayo ndicho chanzo cha unene wa mwili.


  • Ulaji wa nyanya fresh kati ya moja au mbili kila siku asubuhi kama kifungua kinywa kwa miezi kadhaa nako kunachangia kupunguza unene, na ni njia salama sana ya kupunguza unene.


  • Kunywa glasi mbili za maji ya uvuguvugu kila siku asubuhi mara baada ya kuamka kunasaidia kupunguza unene.

Aidha mtu mnene anaweza kutumia diet rahisi ifuatayo ili kupunguza unene;




  1. Asubuhi, kunywa juisi ya matunda fresh au kula matunda na kipande cha mkate usiopakwa siagi.


  2. Mchana, kula vegetable salad na slice 2 za mkate pamoja na matunda au juisi.


  3. Usiku, kula fruit salad au supu ya mbogamboga.

Hakikisha ratiba hiyo inafuatwa kila siku na acha kabisa kutumia vyakula vingine vyenye asili ya mafuta kama vile nyama.


Nadhani kwa hayo machache yanaweza kusaidia. Nimeona niwawekee diet ambayo ni rahisi kupatikana na kutengeneza kwa gharama nafuu.


Asante.


2flag.

Tuesday, September 2, 2008

SIJUI KWA NINI NINAKUWA MNENE WAKATI NINAKULA KIDOGO


Jamani habari za kushinda au kushindwa! Nasema hivyo kwani siyo watu wote wanaoshinda bali wapo walio wengi katika kasi hii wanashindwa ila hawana mahali pa kulalamikia.


Leo ninakuja na ile mada yetu juu ya unene, kitambi au kuwa na uzito mwingi mwilini. Wapo watu ambao wamekuwa wakilalamika na kusema kuwa " Jamani hata sijui kwa nini ninakuwa mnene wakati ninajitahidi kula kidogo au kujinyima mlo wa mchana pamoja na kufanya mazoezi". Watu wengi wanadhani kula sana ndiyo kunasababisha unene. Kumbe, hicho pekee siyo chanzo cha tatizo. Kwani miongoni mwetu tunawajua watu wembamba ambao wanakula sana lakini wanabaki na wembamba wao. Wengine wamekuwa wakila sana ili kuutafuta unene lakini hawanenepi.


Hivyo, licha ya chakula zipo sababu zingine zinazosababisha unene kwani wataalamu mbalimbali wamejaribu kutafiti chanzo cha unene lakini wameshindwa kupata jibu sahihi. Siyo watu wote wanaopata unene kwa kula vyakula, na sababu ya tofauti hizo bado kujulikana. Zifuatazo ni baadhi ya vyanzo vya unene:



  1. Kurithi: Wapo watu ambao wamerithi unene kutoka kwa mababu au wazazi ambapo kunakuwa na uhusiano fulani wa kizazi hicho unaofanana na ulaji wa vyakula fulani. Mtoto ambaye wazazi wake ni wanene ana uwezekano wa asilimia 80 ya yeye pia kuwa mnene kwani inasadikika kuwa hata yeye atakula kama wazazi wake.


  2. Sababu binafsi: Hii inatokana na sababu za kihomoni ambapo zipo homoni mwilini zinazochangia kuzalishwa kwa mafuta kwa wingi mwilini ambayo yanasababisha unene.


  3. Hupungufu wa joto mwilini: Inasemekana kuwa watu wanene wana joto kidogo mwilini kitu kinachochangia kutokutumika vizuri kwa calories zilizozalishwa mwilini, kwani calories zisizotumika zinabadilishwa na kuwa mafuta ambayo ndiyo chanzo cha unene. Joto jingi mwilini linasaidia kuchoma vizuri calories na kufanya mwili kukosa kutengeneza akiba ya mafuta. Kinyume na watu wanene, watu wembamba wanasemekana kuwa na joto jingi linalochoma vizuri calories na kuzifanya zitumike vizuri pasipo kubaki akiba ya mafuta mwilini. Ndiyo maana watu wanene wanashauriwa kufanya mazoezi ili kuzalisha joto la kutosha mwilini ili kuchoma akiba ya mafuta iliyopo mwilini.


  4. Kuhisi njaa mapema na kuwa na hamu ya kula: Inasemekana watu wanene wanahisi njaa mapema na wanakuwa na hamu ya kula ili kuponya njaa yao tofauti na watu wembamba. Aidha miili mikubwa inahitaji chakula kingi ili kutosheleza mahitaji ya miili hiyo.


  5. Uvivu: Pia imebainika kuwa watu wanene ni wavivu wa kufanya shughuli zinazotumia nguvu nyingi ikiwamo mazoezi. Hali hiyo inawafanya waendelee kuhifadhi akiba nyingi ya mafuta mwilini yanayoongeza unene.

JE KIFANYIKE NINI ILI KUONDOKANA NA HALI YA UNENE?


Ungana nami katika mwendelezo wa mada hii.


ASANTE.


2FLAG

Monday, September 1, 2008

KAZI YA VIRUTUBISHO VYA KAROTI


Kama tulivyotangulia kuona zao la karoti na matumizi yake, leo nitaelezea japo kwa ufupi kazi ya virutubisho vinavyopatikana kwenye zao hilo. Virutubisho hivyo ni vifuatavyo:



  1. Vitamini A (Beta - Carotene); hii ni vitamini inayotokana na kirutubisho kinachojulikana kama beta - carotene ambapo mwili hukibadilisha kuwa vitamini A pindi kiingiapo mwilini. Kazi kubwa ya kirutubisho hiki ni kutengeneza retina, kiungo ambacho kipo ndani ya jicho ambapo jicho linapewa uwezo wa kuona vizuri hasa kwenye mwanga hafifu. Kwa wale wenye matatizo ya kuona gizani, yaani night blindness wanashauriwa kula karoti kwa wingi. Pia kirutubisho hiki kinasaidia kutengeneza chembe (cell) kwa ajili ya ngozi, kinywa, macho, na viungo vingine laini ndani ya mwili. Aidha beta - carotene hupunguza uwezekano wa mwili kupatwa na magonjwa ya kansa kwa kuwa na uwezo mkubwa wa kupigana na magonjwa ya aina hiyo. Inasemekana kuwa wavutaji wa sigara wanaokula karoti kwa wingi wanapunguza uwezekano wa kupatwa na magonjwa ya kansa kwenye mapafu kuliko wale ambao wanakula kidogo au hawali kabisa.


  2. Fiber, hii inasaidia kulainisha choo na hata kukinga kuta za utumbo.


  3. Kuna kitu kinaitwa essential oil ambapo kazi yake kubwa ni kupigana na vijidudu tumboni.

Hivyo basi, ulaji wa karoti unaweza kuboresha afya yako na kujikinga na maradhi mbalimbali ambayo yanaweza kukugharimu pindi unapoyapata. Ni vema ukajijengea tabia ya kula karoti japo moja kwa siku, kwani zinapatikana kwa urahisi kabisa na ni kwa pesa kidogo tu.


Mada ijayo nitajibu maombi ya wadau waliotaka niwapatie japo ushauri wa kupunguza vitambi vyao ambavyo leo vimekuwa kero kwao na kusababisha washindwe kufanya kazi nyingine kwa umahiri kabisa.


KILA LA HERI, TUONANE SIKU HIYO, MUNGU AKIPENDA.


2FLAG.