Tuesday, September 2, 2008

SIJUI KWA NINI NINAKUWA MNENE WAKATI NINAKULA KIDOGO


Jamani habari za kushinda au kushindwa! Nasema hivyo kwani siyo watu wote wanaoshinda bali wapo walio wengi katika kasi hii wanashindwa ila hawana mahali pa kulalamikia.


Leo ninakuja na ile mada yetu juu ya unene, kitambi au kuwa na uzito mwingi mwilini. Wapo watu ambao wamekuwa wakilalamika na kusema kuwa " Jamani hata sijui kwa nini ninakuwa mnene wakati ninajitahidi kula kidogo au kujinyima mlo wa mchana pamoja na kufanya mazoezi". Watu wengi wanadhani kula sana ndiyo kunasababisha unene. Kumbe, hicho pekee siyo chanzo cha tatizo. Kwani miongoni mwetu tunawajua watu wembamba ambao wanakula sana lakini wanabaki na wembamba wao. Wengine wamekuwa wakila sana ili kuutafuta unene lakini hawanenepi.


Hivyo, licha ya chakula zipo sababu zingine zinazosababisha unene kwani wataalamu mbalimbali wamejaribu kutafiti chanzo cha unene lakini wameshindwa kupata jibu sahihi. Siyo watu wote wanaopata unene kwa kula vyakula, na sababu ya tofauti hizo bado kujulikana. Zifuatazo ni baadhi ya vyanzo vya unene:



  1. Kurithi: Wapo watu ambao wamerithi unene kutoka kwa mababu au wazazi ambapo kunakuwa na uhusiano fulani wa kizazi hicho unaofanana na ulaji wa vyakula fulani. Mtoto ambaye wazazi wake ni wanene ana uwezekano wa asilimia 80 ya yeye pia kuwa mnene kwani inasadikika kuwa hata yeye atakula kama wazazi wake.


  2. Sababu binafsi: Hii inatokana na sababu za kihomoni ambapo zipo homoni mwilini zinazochangia kuzalishwa kwa mafuta kwa wingi mwilini ambayo yanasababisha unene.


  3. Hupungufu wa joto mwilini: Inasemekana kuwa watu wanene wana joto kidogo mwilini kitu kinachochangia kutokutumika vizuri kwa calories zilizozalishwa mwilini, kwani calories zisizotumika zinabadilishwa na kuwa mafuta ambayo ndiyo chanzo cha unene. Joto jingi mwilini linasaidia kuchoma vizuri calories na kufanya mwili kukosa kutengeneza akiba ya mafuta. Kinyume na watu wanene, watu wembamba wanasemekana kuwa na joto jingi linalochoma vizuri calories na kuzifanya zitumike vizuri pasipo kubaki akiba ya mafuta mwilini. Ndiyo maana watu wanene wanashauriwa kufanya mazoezi ili kuzalisha joto la kutosha mwilini ili kuchoma akiba ya mafuta iliyopo mwilini.


  4. Kuhisi njaa mapema na kuwa na hamu ya kula: Inasemekana watu wanene wanahisi njaa mapema na wanakuwa na hamu ya kula ili kuponya njaa yao tofauti na watu wembamba. Aidha miili mikubwa inahitaji chakula kingi ili kutosheleza mahitaji ya miili hiyo.


  5. Uvivu: Pia imebainika kuwa watu wanene ni wavivu wa kufanya shughuli zinazotumia nguvu nyingi ikiwamo mazoezi. Hali hiyo inawafanya waendelee kuhifadhi akiba nyingi ya mafuta mwilini yanayoongeza unene.

JE KIFANYIKE NINI ILI KUONDOKANA NA HALI YA UNENE?


Ungana nami katika mwendelezo wa mada hii.


ASANTE.


2FLAG

No comments: