Habari za siku wadau wa blog hii. Ni matumaini yangu kuwa mnaendelea vizuri katika shughulimbalimbali za kujitafutia riziki na maendeleo. Ningependa nikiri na kuwaomba radhi kwa ukimya wangu unaojitokeza mara kwa mara.
Leo nimeona nijibu baadhi ya maombi ya wasomaji wangu waliotaka kufahamu aina ya juisi mbalimbali na jinsi zinavyotengenezwa. Binafsi nimeona niwaongezee na kipengele kingine cha faida za juisi hizo katika mwili wa binadamu.
Zipo juisi za namna tofauti na matumizi yake yanategemea na malengo ya mtumiaji. Nadhani watumiaji wengi wanakunywa juisi bila kujua umuhimu au kazi yake mwilini. Wengi hawajui ni juisi gani itumike wakati gani.
Hebu fuatilia aina zifuatazo na upate kujua utengenezaji wake na kazi zake.
- JUISI YA KAROTI NA APPLE: Chukua kiasi cha karoti na apple kinachotosha kutengeneza juisi kwa kiasi ulichokusudia. Usikose kipande cha limao kiasi cha nusu. Anza kuandaa juisi yako kwa kuosha na kumenya karoti na apple kisha katakata katika vipande vidogo vinavyoweza kusagika kirahisi kwenye blenda. Saga mchanganyiko wako ili upate juisi. Baada ya kupata mchanganyiko wa juisi yako kamulia limao kwa ajili ya kuongeza ladha. Unaweza kuiweka kwenye friji ili ipate ubaridi kidogo na tayari kwa kuinywa. Siyo lazima kuongeza sukari kwenye juisi kwani matunda yana sukari asilia.
- JUISI YA KAROTI NA APPLE ina uwezo wa kutunza ngozi kwani tunda la apple linaondoa uchafu kwenye ngozi na karoti nayo kwa kutumia kirutubisho cha beta-karotini chenye uwezo wa kutengeneza Vitamin A hulinda na kurejesha uhai katika ngozi ambapo inaifanya ionekane nyororo. Pia juisi hii husafisha tumbo na kuondoa uchafu tumboni. Aidha juisi hii inafanya ini lifanye kazi yake vizuri kwa kulainisha nyongo na kusaidia kuondoa uchafu.
- JUISI YA VIAZI MVIRINGO: Chukua viazi mviringo vinavyotosha kwa juisi. Andaa kwa kuviosha na kumenya kisha katakata vipande vidogo kwa ajili ya kuvisaga. Saga ili upate juisi uliyoikusudia.
- JUISI YA VIAZI MVIRINGO inatumika kama dawa ya kuondoa au kupunguza asidi au gesi tumboni. Juisi ya viazi mviringo inaweza kusaidia kupunguza matatizo ya figo, kisukari, unene au kitambi.
- JUISI YA MBOGAMBOGA: Juisi hii ina mchanganyiko wa mbogamboga kam vile karoti, nyanya na matango. Maandalizi yake ni kam juisi nyingine. Anza kwa kuosha kisha kumenya na kukatakata vipande. Saga mchanganyiko huo kwenye blenda ili upate juisi uliyoikusudia. Unaweza kuweka kwenye friji ili ipate ubaridi kidogo.
- JUISI hii inasadaidia kuzuia kansa hasa ile ya kwenye mfumo wa kumeng`enya chakula, kukinga mapafu na artery. Pia inasaidia kuimarisha kinga.
- JUISI YA TIKITI MAJI: Chukua tikiti maji (watermelon) na osha kisha likate vipande na chukua nyama yake ya ndani ambayo utaisaga na kupata juisi.
- JUISI YA TIKITI MAJI ina uwezo wa kusafisha figo pamoja na njia ya mkojo. Inazuia unene kwa kuwa na kiwango kidogo cha calories.
KWA aina hizo chache za juisi unaweza kujua umuhimu wa juisi za matunda na mbogamboga tunazotumia. Kwa leo ninaishia hapo na siku zijazo nitaendelea kukupatia ufahamu kwa aina zingine za juisi pamoja na kazi zake.
SIKU NJEMA.
No comments:
Post a Comment