Thursday, September 18, 2008

UPUNGUFU WA NGUVU ZA KIUME (SEXUAL IMPOTENCE)

Hongera kwa saumu kwa wale waliofunga, na wale wenzangu na mie habari za siku tele. Ndugu zangu msidhani kama niliingia mitini bali dharura za kimaisha zilinizonga. Leo naomba nizungumzie kuhusu suala nyeti la upungufu wa nguvu za kiume na namna ambavyo mtu mwenye tatizo kama hili anaweza kutumia ushauri wangu ili kurejesha heshima yake katika kufanya mambo ya kikubwa. Hapo awali inasemekana tatizo hili lilisababishwa na sababu za kisaikolojia pamoja na uzee au umri mkubwa ambapo viungo vya mwili vinakuwa vimechoka.
Kwa miaka ya hivi karibuni imebainika kuwa sababu zinazosababisha upungufu wa nguvu za kiume zimeongezeka na zifuatazo ni baadhi ya sababu hizo, nazo ni;
  • Kutokana na mabadiliko ya kisayansi na kukua kwa teknolojia wanaume wengi wamekuwa wakiishi maisha rahisi ya kutotumia miili yao kwa kufanya kazi zinazotumia nguvu na matokeo yake mwili unashindwa kujenga misuli imara katika viungo mbalimbali vya mwili.
  • Ulaji wa vyakula vilivyopitia viwandani na vyenye asili ya mafuta na protini nyingi ambapo vyakula hivyo vinakosa virutubisho muhimu kwa ajili ya kuimarisha viungo nyeti. Vyakula vyenye asili ya mafuta vinasababisha kuwepo kwa cholestral kwenye damu ambayo inapunguza au kuzuia mzunguko wa damu kwenye nyeti za mwanaume na hatimaye kushindwa kufanya kazi vizuri.
  • Matumizi ya mara kwa mara ya vileo/pombe, kahawa, uvutaji wa sigara nayo yanachangia upungufu wa nguvu za kiume.
  • Athari za magonjwa kama kisukari, arteri, magonjwa ya neva yanayosababishwa na ulaji wa vyakula vyenye protini nyingi na mafuta mengi.
  • Ukosefu wa madini na vitamini mbalimbali zinazopatikana kwa wingi kutoka kwenye matunda na mbogamboga.

Kutokana na kero ya tatizo la upungufu wa nguvu za kiume au uhanithi, watu wengi wamekuwa wakijaribu kutumia vidonge ili waweze kuongeza nguvu na kufurahia tendo la ndoa. Imebainika kuwa matumizi ya vidonge hivyo yana madhara kwa afya ya mtumiaji. Baadhi ya athari anazoweza kuzipata mtumiaji wa dawa hizo ni pamoja na kuharisha, kichefuchefu, kuumwa na kichwa, kupooza baadhi ya viungo, upofu, kutosikia, na hata kupoteza kabisa kwa nguvu za kiume. Hali hiyo imewafanya watu wengi siku hizi wageukie matumizi ya dawa za mimea asilia au vyakula asilia ambapo havina athari kwa mtumiaji.

Hivyo basi mtu mwenye tatizo la uhanithi au upungufu wa nguvu za kiume anapaswa kuzingatia yafuatayo:

  • Kutumia kwa wingi matunda ikiwa kama sehemu ya mlo wake kila wakati anapopata mlo kwa siku tano hadi saba za mwanzo. Mtumiaji anaweza kuwa na milo mitatu kwa siku ambapo pia matumizi ya juisi ya zabibu, machungwa, apple, peas, nanasi, parachichi na tikitiki maji yanahimizwa.
  • Matumizi ya vyakula vya nafaka pia yanafufua matumaini kwa mtu aliyepoteza uweza wa kufanya tendo la ndoa kuweza kusimama upya. Inashauriwa pia mtumiaji atumie asali, mtindi, kitunguu saumu, mbogamboga na matunda mara kwa mara. Wakati huo huo mgonjwa aepuke matumizi ya sigara, pombe au vileo, kahawa, na vyakula vilivyopitia viwandani na vyenye protini na mafuta mengi.
  • Mazoezi ya viungo au mwili ama kufanya kazi zinazotumia nguvu nako kunasaidia kuimarisha viungo vya mwili. Iwapo mgonjwa atafanya kazi ya kutumia nguvu au mazoezi ya viungo japo dakika 30 hadi 45 kila siku na kisha kula vyakula vilivyoelezewa hapo juu anaweza kuwa na uwezo wa kusimama mwenyewe pasipo kutumia msaada wa vidonge vya kuongeza nguvu.

Pamoja na hayo machache mada ijayo nitaendeleza kutaja baadhi ya vyakula, matunda na matumizi ya mbogamboga na kazi zake katika kufufua uwezo wa wanaume aliyepoteza nguvu za kiume.

KILA LA KHERI.

2Flag.

Wednesday, September 10, 2008

SAMAHANI WANABLOG

Napenda kuwaomba samahani wanablog kwasababu nimekuwa kimya kwa muda sasa. Sababu mojawapo ni kwamba kwa kipindi kisichopungua wiki moja iliyopita nilikuwa na dharura kiasi ambacho nimeshindwa kuwawekea matoleo mapya kwenye blog hii. Hata hivyo, hali hiyo inaweza kuendelea kwa siku kadhaa na pindi nitakapomaliza dharura zangu nitaendelea kuwapatia mada mbalimbali kama kawaida. Naomba uvumilivu wenu, tafadhali.

2flag.

Wednesday, September 3, 2008

JINSI YA KUPUNGUZA UNENE


Za leo! Mambo vipi! Hizi ndizo salamu za siku hizi hasa kwa vijana. Baada ya salamu hiyo naomba turudi kwenye mada ya leo ya jinsi ya kupunguza unene. Kwanza kabisa napenda kuwashauri watu wanene wasitumie vidonge/madawa ya kiwandani kwa lengo la kupunguza unene, kwani vidonge vina athari zake mwilini ukizingatia kuwa vina kemikali ambazo baadhi hubakia mwilini na kutengeneza sumu.


Watu wanashauriwa kutumia vitamini itokanayo na matunda na mbogamboga. Aidha, kwa mtu mnene kushinda na njaa siyo dawa au tiba sahihi ya kupunguza unene. Mtu anayetaka kupunguza unene/uzito ni vema akazingatia misingi ifuatayo:



  • Punguza kula chumvi nyingi maana chumvi inatunza maji mwilini ambayo pia yana mchango mkubwa katika kuongeza uzito wa mwili. Kwa kuacha kula chumvi nyingi maji yataweza kupungua mwilini kwa njia ya mkojo au jasho.


  • Ongeza kula vyakula vyenye madini ya potasium, calcium, na magnesium ambapo madini hayo yanapatikana kutoka kwenye mbogamboga mbichi na matunda au maziwa ya soya.


  • Kula vyakula vyenye wanga, punguza vyakula vyenye mafuta na protini.


  • Kunywa maji mengi kiasi cha lita 2 kwa siku na kwa kila siku.


  • Fanya mazoezi ya mwili/viungo japo kwa dakika 30 hadi 60 kila asubuhi. Kutembea ni mojawapo ya mazoezi.

Katika kuongezea vitu hivyo hapo juu, mlengwa anashauriwa pia kutumia;




  • Asali kijiko kimoja na kuchanganya nusu ndimu au limao kwenye maji yenye uvuguvugu kiasi cha glasi moja na kunywa mara kwa mara.


  • Matumizi ya cabbage pia yamethibitika kuwa na mchango mkubwa katika kupunguza unene kwani kemikali zilizomo ndani yake zinasaidia kuzuia wanga na sukari kubadilishwa kimfumo na kuwa mafuta ambayo ndicho chanzo cha unene wa mwili.


  • Ulaji wa nyanya fresh kati ya moja au mbili kila siku asubuhi kama kifungua kinywa kwa miezi kadhaa nako kunachangia kupunguza unene, na ni njia salama sana ya kupunguza unene.


  • Kunywa glasi mbili za maji ya uvuguvugu kila siku asubuhi mara baada ya kuamka kunasaidia kupunguza unene.

Aidha mtu mnene anaweza kutumia diet rahisi ifuatayo ili kupunguza unene;




  1. Asubuhi, kunywa juisi ya matunda fresh au kula matunda na kipande cha mkate usiopakwa siagi.


  2. Mchana, kula vegetable salad na slice 2 za mkate pamoja na matunda au juisi.


  3. Usiku, kula fruit salad au supu ya mbogamboga.

Hakikisha ratiba hiyo inafuatwa kila siku na acha kabisa kutumia vyakula vingine vyenye asili ya mafuta kama vile nyama.


Nadhani kwa hayo machache yanaweza kusaidia. Nimeona niwawekee diet ambayo ni rahisi kupatikana na kutengeneza kwa gharama nafuu.


Asante.


2flag.

Tuesday, September 2, 2008

SIJUI KWA NINI NINAKUWA MNENE WAKATI NINAKULA KIDOGO


Jamani habari za kushinda au kushindwa! Nasema hivyo kwani siyo watu wote wanaoshinda bali wapo walio wengi katika kasi hii wanashindwa ila hawana mahali pa kulalamikia.


Leo ninakuja na ile mada yetu juu ya unene, kitambi au kuwa na uzito mwingi mwilini. Wapo watu ambao wamekuwa wakilalamika na kusema kuwa " Jamani hata sijui kwa nini ninakuwa mnene wakati ninajitahidi kula kidogo au kujinyima mlo wa mchana pamoja na kufanya mazoezi". Watu wengi wanadhani kula sana ndiyo kunasababisha unene. Kumbe, hicho pekee siyo chanzo cha tatizo. Kwani miongoni mwetu tunawajua watu wembamba ambao wanakula sana lakini wanabaki na wembamba wao. Wengine wamekuwa wakila sana ili kuutafuta unene lakini hawanenepi.


Hivyo, licha ya chakula zipo sababu zingine zinazosababisha unene kwani wataalamu mbalimbali wamejaribu kutafiti chanzo cha unene lakini wameshindwa kupata jibu sahihi. Siyo watu wote wanaopata unene kwa kula vyakula, na sababu ya tofauti hizo bado kujulikana. Zifuatazo ni baadhi ya vyanzo vya unene:



  1. Kurithi: Wapo watu ambao wamerithi unene kutoka kwa mababu au wazazi ambapo kunakuwa na uhusiano fulani wa kizazi hicho unaofanana na ulaji wa vyakula fulani. Mtoto ambaye wazazi wake ni wanene ana uwezekano wa asilimia 80 ya yeye pia kuwa mnene kwani inasadikika kuwa hata yeye atakula kama wazazi wake.


  2. Sababu binafsi: Hii inatokana na sababu za kihomoni ambapo zipo homoni mwilini zinazochangia kuzalishwa kwa mafuta kwa wingi mwilini ambayo yanasababisha unene.


  3. Hupungufu wa joto mwilini: Inasemekana kuwa watu wanene wana joto kidogo mwilini kitu kinachochangia kutokutumika vizuri kwa calories zilizozalishwa mwilini, kwani calories zisizotumika zinabadilishwa na kuwa mafuta ambayo ndiyo chanzo cha unene. Joto jingi mwilini linasaidia kuchoma vizuri calories na kufanya mwili kukosa kutengeneza akiba ya mafuta. Kinyume na watu wanene, watu wembamba wanasemekana kuwa na joto jingi linalochoma vizuri calories na kuzifanya zitumike vizuri pasipo kubaki akiba ya mafuta mwilini. Ndiyo maana watu wanene wanashauriwa kufanya mazoezi ili kuzalisha joto la kutosha mwilini ili kuchoma akiba ya mafuta iliyopo mwilini.


  4. Kuhisi njaa mapema na kuwa na hamu ya kula: Inasemekana watu wanene wanahisi njaa mapema na wanakuwa na hamu ya kula ili kuponya njaa yao tofauti na watu wembamba. Aidha miili mikubwa inahitaji chakula kingi ili kutosheleza mahitaji ya miili hiyo.


  5. Uvivu: Pia imebainika kuwa watu wanene ni wavivu wa kufanya shughuli zinazotumia nguvu nyingi ikiwamo mazoezi. Hali hiyo inawafanya waendelee kuhifadhi akiba nyingi ya mafuta mwilini yanayoongeza unene.

JE KIFANYIKE NINI ILI KUONDOKANA NA HALI YA UNENE?


Ungana nami katika mwendelezo wa mada hii.


ASANTE.


2FLAG

Monday, September 1, 2008

KAZI YA VIRUTUBISHO VYA KAROTI


Kama tulivyotangulia kuona zao la karoti na matumizi yake, leo nitaelezea japo kwa ufupi kazi ya virutubisho vinavyopatikana kwenye zao hilo. Virutubisho hivyo ni vifuatavyo:



  1. Vitamini A (Beta - Carotene); hii ni vitamini inayotokana na kirutubisho kinachojulikana kama beta - carotene ambapo mwili hukibadilisha kuwa vitamini A pindi kiingiapo mwilini. Kazi kubwa ya kirutubisho hiki ni kutengeneza retina, kiungo ambacho kipo ndani ya jicho ambapo jicho linapewa uwezo wa kuona vizuri hasa kwenye mwanga hafifu. Kwa wale wenye matatizo ya kuona gizani, yaani night blindness wanashauriwa kula karoti kwa wingi. Pia kirutubisho hiki kinasaidia kutengeneza chembe (cell) kwa ajili ya ngozi, kinywa, macho, na viungo vingine laini ndani ya mwili. Aidha beta - carotene hupunguza uwezekano wa mwili kupatwa na magonjwa ya kansa kwa kuwa na uwezo mkubwa wa kupigana na magonjwa ya aina hiyo. Inasemekana kuwa wavutaji wa sigara wanaokula karoti kwa wingi wanapunguza uwezekano wa kupatwa na magonjwa ya kansa kwenye mapafu kuliko wale ambao wanakula kidogo au hawali kabisa.


  2. Fiber, hii inasaidia kulainisha choo na hata kukinga kuta za utumbo.


  3. Kuna kitu kinaitwa essential oil ambapo kazi yake kubwa ni kupigana na vijidudu tumboni.

Hivyo basi, ulaji wa karoti unaweza kuboresha afya yako na kujikinga na maradhi mbalimbali ambayo yanaweza kukugharimu pindi unapoyapata. Ni vema ukajijengea tabia ya kula karoti japo moja kwa siku, kwani zinapatikana kwa urahisi kabisa na ni kwa pesa kidogo tu.


Mada ijayo nitajibu maombi ya wadau waliotaka niwapatie japo ushauri wa kupunguza vitambi vyao ambavyo leo vimekuwa kero kwao na kusababisha washindwe kufanya kazi nyingine kwa umahiri kabisa.


KILA LA HERI, TUONANE SIKU HIYO, MUNGU AKIPENDA.


2FLAG.



Friday, August 29, 2008

IJUE KAROTI NA FAIDA ZAKE

Habari za maisha wadau wenzangu! Naomba leo niwape japo kidogo kuhusu matumizi ya zao la karoti pamoja na faida zinazopatikana kutokana na utumiaji wa zao hilo, ambalo kimsingi mizizi yake ndiyo hasa zao lenyewe. Napenda niwaombe radhi wale ndugu zangu waliouliza maswali juu ya kujikinga ama namna ya kuondokana na unene. Mada inayohusu unene na athari zake nitaitoa wiki ijayo na nitakupa dokezo ambazo zitakusaidia kuondokana na unene au kitambi.

Tukirudi kwenye mada ya leo, kumbuka kuwa karoti inalimwa karibu kila pembe ya dunia hii. Zao hili linatofautiana katika rangi, kwani kuna karoti nyeusi, zenye rangi ya pinki, nyekundu na njano. Karoti yenye rangi nyekundu na njano ndiyo hasa tunayolima hapa TZ. Karoti za rangi nyekundu na njano ndizo zinasemekana kuwa na virutubisho vingi sana kuliko karoti nyingine.

Karoti ina protini kidogo na haina mafuta kama tulivyoona kwa tunda la avocado. Pia ina asili ya wanga, na ni chanzo kizuri cha vitamini B, C na E. Aidha ina madini mengi ikiwemo madini ya chuma. Kuna kitu kinaitwa beta-carotene ambayo imo ndani ya karoti na hii ikiingia mwilini inabadilishwa na kuwa vitamini A. Vile vile karoti ina kirutubisho kinachoitwa fiber ambacho ni muhimu kwa kukinga kuta za utumbo.
Karoti ikitumiwa vizuri na tena mara kwa mara inasaidia kukinga na kuponya magonjwa yafuatayo: macho hasa kutoona gizani au kwenye mwanga hafifu, ngozi, kupunguza tindikali inayodhuru tumboni na kukinga magonjwa yenye asili ya kansa.


Karoti inaweza kuliwa kwa namna mbalimbali kama vile, ikiwa mbichi kwa kutafuna, inaweza kupikwa na kuchanganywa na mbogamboga zingine, inaweza kusagwa na kupata juisi ambayo pia inaweza kuchanganywa na juisi zingine, aidha kukatwakatwa na kuchanganywa kwenye salad ya matunda au mbogamboga. Machicha ya karoti iliyosagwa yanaweza kutumika kama dawa kukinga ama kuponya maradhi ya nje ya mwili.
Mada nyingine nitazungumzuzia kazi ya virutubisho vilivyomo ndani ya karoti.

KILA LA HERI NA TUONANE SIKU NYINGINE MUNGU AKIPENDA.

Wednesday, August 27, 2008

JE, NITAKULA NINI AU UTAKULA NINI NA KWA KIASI GANI?


Habari za mihangaiko wadau wenzangu! Hongereni kwa kazi. Nasema hongera kwa kazi na siyo pole kwa kazi kwani viongozi wetu wametuhasa tuseme hongera badala ya pole. Maana pole anapewa mtu mwenye matatizo. Nasema hivyo kwa sababu kazi siyo matatizo ila ukikosa kazi ndipo matatizo mengi hujitokeza.


Nawashukuru wadau wenzangu kwani nimepokea baadhi ya maoni na maswali kutoka kwa wasomaji wakitaka kujua watumie chakula gani, kwa kiwango ama kiasi gani, katika muda gani, na kwa wale ambao walishakula sana vyakula nilivyovitaja katika mada yangu iliyotangulia juu ya dokezo la EAT AT YOUR OWN RISK, wafanye nini ili kuepuka kupatwa maradhi yanayosababishwa na ulaji wa vyakula hivyo.


Jibu rahisi ambalo naweza kukupatia kwa haraka nitakuambia kula kulingana na mahitaji ya mwili wako. Lakini, je, utajuaje mahitaji ya mwili wako? Mdau mwenzangu nitakuomba tuendelee kuwa pamoja maana zipo mada maalum zitakazojibu maswali hayo yote kwa ufasaha. Hata kama umekula sana vyakula hivyo na ukajihisi kuwa ni mnene, blog hii itakupatia fomula mbalimbali ambazo unaweza kuzitumia kupunguza unene.


Kwa ufupi rejea kwenye hilo jedwali hapo juu la mpangilio wa vyakula. Kwa wale wasomi wa lugha ya wenzetu wanaliita "A Pyramid of Balanced Diet". Jedwali hilo linakupa namna ambavyo unaweza kupangilia mlo wako wa kila siku, na kula chakula unachopaswa kula kwa kiasi na kiwango unachotaka kwa afya yako. Kwa mfano ukianzia chini ambako nafasi ni pana inamaanisha unatakiwa ule kwa wingi vyakula hivyo na kwa kadri unavyopanda juu unashauriwa upunguze kula chakula kilichoelezwa katika makundi hayo ya vyakula.



  1. Unashauriwa ule kwa wingi vyakula vya nafaka kama wali, ugali, mkate n.k, ingawa hapa watu wengine hawataki kabisa kusikia habari za ugali labda wale watu waliokulia bara.


  2. Kula kwa wingi vyakula vya mbogamboga na matunda maana yakula hivi vina virutubisho vyote na ni kinga na dawa kwa baadhi ya maradhi mwilini .


  3. Kula kwa kiasi kidogo vyakula vyenye protini nyingi hasa vile vinavyotokana na mazao ya wanyama kama vile; nyama, kuku, mayai, maziwa, mtindi, samaki na maharage makavu n.k, ukiweza kula vyakula vya aina hii mara moja kwa wiki.


  4. Ukiweza, acha kabisa ama kula kidogo sana vyakula vyenye asili ya mafuta ama vilivyoongezwa mafuta, vilivyoongezwa sukari. Najua wengi wanapenda kula vyakula vilivyokaangizwa, ukiwaambia wapike ama wale chukuchuku wanakujibu kwani nina shida gani, raha jipe mwenyewe, kumbe hawajui ndiyo kwanza wanatengeneza shida zitakazowapa karaha badala ya raha.

Najua ni vigumu kwa watu kufuata mpangilio huu. Lakini kama umedhamiria kuilinda afya yako unaweza na tena vyakula hivyo ni rahisi kuvipata katika masoko yetu hapa nchini TZ tofauti na wenzetu kule majuu.


Aidha niliposema kula kulingana na mahitaji ya mwili wako, unapaswa kujua wewe mwenyewe unafanya shughuli gani. Kwasababu, mahitaji ya miili yanatofautiana kulingana na aina ya shughuli au kazi ya mtu husika. Kwa mfano watu wanaofanya kazi maofisini na walimu wanahitaji kiasi kidogo cha chakula; kwa wanafunzi na wafanyabiashara na wachuuzi pamoja na watumishi wa kazi za ndani wanahitaji nyongeza kidogo tofauti na mtu wa ofisini; mafundi kama seremala, umeme, watumishi wa nyumbani wanaofanya kazi kama za kulisha mifugo na nyingine ngumu wanahitaji chakula cha kutosha; na wafanyakazi wa ujenzi kama wabeba zege, ujenzi wa barabara, migodini, wanariadha na wengine wa aina hiyo wanahitaji chakula kingi ili kutosheleza mahitaji ya miili yao kwani wao wanatumia calories nyingi. Hivyo ni vema ukazingatia hilo ili usije kula chakula zaidi ya mahitaji ya mwili wako na matokeo yake ni unene unaoweza kukusababishia matatizo au hata usipokuwa mnene unaweza kujikuta unapata kisukari kinyume na matarajio yako.


Kwa maelezo hayo nadhani nitakuwa nimejibu baadhi ya maswali ya wasomaji waliotaka kujua watakula nini, kwa kiasi na kiwango gani na wakati gani. Kumbuka, hapo baadaye nitakupa jinsi unavyotakiwa kupangilia milo yako kwa siku. Kama una maswali zaidi usisite kuuliza.


Asante kwa ushirikiano wenu na karibu tena.





Tuesday, August 26, 2008

DOKEZO JUU YA MANENO "EAT AT YOUR OWN RISK"

Je, unafahamu kuwa watu tulio wengi tunachimbia makaburi yetu wenyewe kwa kutumia mikono, vijiko, visu na uma? Ni kwa nini nasema hivyo, kwasababu watu wengi tunapenda kula kila kitu kizuri tunachokiona kwa macho yetu na chenye ladha ulimini bila kujali athari za chakula chenyewe katika miili yetu. Tunakula vyakula vyenye sukari nyingi, mahanjumati yaliyokaangizwa kwa mafuta tusiyoyajua vizuri, chumvi nyingi ili tufurahishe ndimi zetu na vingine vingi vya namna hiyo kama wale wenzangu na mimi tunaopenda kwenda kujipumzisha ifikapo jioni au weekend katika maeneo fulani ya vimiminika huku tukipata nyama choma au kitimoto kwa wale walioamua kufumba macho.

Kumbuka, vyakula nilivyojaribu kuvitaja kwa uchache hapo juu ndiyo chanzo cha maradhi mbalimbali mwilini. Magonjwa ambayo ni rahisi kuyapata kutokana na ulaji wa vyakula kama hivyo ni artery, stroke, magonjwa yote ya moyo, kisukari, unene au kitambi ingawa watu wachache wanaipendelea hali hiyo ili nao waitwe au wafanane na mafisadi, na aina mbalimbali za magonjwa ya kansa.
Hebu fikiria, magonjwa mengi yamekuwa yakisababishwa na vimelea au wadudu mbalimbali wa magonjwa, lakini magonjwa niliyoyataja hapo juu hayahusiani na mdudu wa magonjwa isipokuwa mdudu wa ugonjwa kama huo ni wewe mwenyewe na chakula unachokula.
Hivyo ni vema kujikinga na vyakula nilivyotangulia kuvitaja kama vile vyenye sukari, vilivyopitia viwandani, vyenye chumvi nyingi, mafuta, protini nyingi, vinywaji baridi kama soda isipokuwa natural juice, vitafunwa au vitu vya kutafunatafuna kama maandazi, keki, donati n.k na pia tuepuke kula ovyo bila mpangilio. Hii ni kwa afya yako na faida yako na jamii inayokuzunguka. Haya, anza sasa, badilika. DON`T RISK YOUR LIFE, tunakupenda na bado tunakuhitaji. Usimtafute mchawi ukasema umerogwa pale utakapoanguka ghafla in case umepatwa na shinikizo la damu.

UMEWAHI KUONA MAANDISHI HAYA MAHALA POPOTE?

Alama hiyo hapo juu na maandishi yake ya PARK AT YOUR OWN RISK siyo ngeni kwani tumekuwa tukikutana nayo sehemu mbalimbali kama vile kwenye majengo ya ibada, kumbi za starehe, sehemu za vinywaji kama vile bar, n.k.
Je, maandishi ya hapo chini umewahi kukutana nayo wapi na yanamaanisha nini? Naomba maoni yako.

EAT AT YOUR OWN RISK



2FLAG




Monday, August 25, 2008

UNAFAHAMU NAMNA UNAVYOWEZA KULA TUNDA LA AVOCADO

Kimsingi avocado au parachichi siyo tunda kama tunavyofikiria bali ni jamii ya mbogamboga. Hii inatokana na ukweli kwamba tunda hilo limekosa baadhi ya vitu vinavyoleta utamu ambavyo vinapatikana kwenye matunda mengine tuliyoyazowea hivyo avocado limekosa sifa ya kuwa katika jamii ya matunda isipokuwa lipo katika jamii ya mbogamboga. Tunda hili linaweza kuandaliwa na kuliwa katika namna tofauti kama ifuatavyo:

  • fruit salad, yaani mchanganyiko wa matunda mbalimbali yaliyoandaliwa kwa kukatwakatwa vipande vidogo na kukamuliwa limao kwa ajili ya kuongeza ladha. Maandalizi ya mchanganyiko huu ni rahisi kwani muandaaji anatakiwa kuchukua avocado na matunda mengine kama vile ndizi, matango, mapapai, zabibu n.k na kisha kuyaosha na kuyamenya ambapo mchanganyiko huo unaweza kuhifadhiwa kwenye jokofu ili upate ubaridi kidogo kabla ya kuliwa. mchanganyiko huu pia unaweza kuongezwa maziwa kama utapenda

  • Vegetable salad, huu ni mchanganyiko wa avocado na jamii ya mbogamboga zilizoandaliwa kwa kukatwakatwa vipande. Mchanganyiko huu unaweza kuhusisha mboga kama nyanya, cabbage, pilipili hoho, n.k. Pia katika mchanganyiko kama huu unaweza kuweka limao ili kuleta ladha fulani mdomoni. Kwa wenzetu hupenda kuweka aina fulani ya mafuta kama vile olive oil ili kuipa ladha zaidi. Lakini kama uwezo wetu hauruhusu mambo hayo basi siyo lazima sana kwani vitu vya msingi utakuwa umevipata. Maandalizi yake hayana tofauti na yale ya fruit salad.

  • Juisi, tunda la avocado ni zuri kwa kutengenezea juisi. Inashauriwa upate avocado lililoiva vizuri ili iwe rahisi kulisaga. Unaweza kutengeneza juisi ya avocado pekee au unaweza kuchanganya na tunda jingine kama vile apple, pensheni, embe n.k. Utengenezaji wa juisi unategemea uwepo wa vifaa kama juicer au blenda. Lakini kama hauna uwezo wa kupata au kununua vitu hivyo ambavyo pia vinatumia umeme, unaweza kutumia kinu kidogo kusaga ili kupata mchanganyiko uliosagika vizuri kisha kupata juisi uliyoikusudia. Wakati mwingine inabidi tukumbuke tulikotoka ambapo wazee wetu walikuwa wanatengeneza dawa za aina hiyo kwa kutumia vifaa hivyo vya asili.

  • Fresh fruit, unaweza kula avocado kama lilivyo kwa kulimenya na kuondoa mbegu yake. Lakini zingatia usafi kabla ya kula tunda hilo usije ukapatwa na maradhi ya tumbo.

  • Avocado linaweza kutengenezwa cream na ikaliwa kama ile uliyozowea kununua kwenye maduka ya Bakhresa. Hii inahitaji hatua fulani ili uweze kupata kitu ulichokikusudia.

  • Avocado linaweza kupakwa kwenye mkate mfano wa siagi. Kama utapenda unaweza kutumia chumvi kidogo ili kuongeza ladha.

Kumbukeni unapoandaa vitu hivyo hapo juu ni lazima uzingatie usafi ukianzia wewe mwenyewe, vyombo utakavyotumia pamoja na matunda, siyo lazima upate matunda yote ili kukamilisha mchanganyiko ulioelezewa hapo juu, bali unaweza kuchukua baadhi kutegemeana na uwezo wako ili mradi tunda la msingi kama avocado lipo kwenye mchanganyiko wako. Matunda haya yapo karibu kila kona za mitaa ya Darisalama kwa wale waliopo jiji hilo, pia yanapatikana baadhi ya mikoa hapa nchini, hivyo siyo mpaka ushauriwe na daktari ndipo ule matunda, anza sasa kula matunda, japo moja kwa siku si haba.

Kwa wale watakaohitaji kujua maandalizi na matumizi ya avocado kwa ajili ya kutunza nywele au ngozi wanaweza kuwasiliana nami kupitia email zifuatazo: larkado@gmail.com au leofiderk@yahoo.com

Asante.

2FLAG









Saturday, August 23, 2008

AVOCADO NA FAIDA ZAKE


Leo napenda niendeleze mada ya tunda la avocado pamoja na faida zake. Kabla ya kuongelea faida zake ningependa nielezee kwanza vitu ama virutubisho vinavyopatikana ndani ya tunda hilo. Vitu hivyo ni kama ifuatavyo;


MAJI: tunda hili lina kiasi kidogo cha maji tofauti na matunda mengine tuliyozoea kula.

MAFUTA: avocado lina kiwango kikubwa cha mafuta na ndani ya kiasi hicho cha mafuta kuna tindikali (acid) mbalimbali zinazosaidia kukinga na kutibu maradhi katika mwili.

PROTINI: tunda hili pia lina kiwango cha juu cha protini kutegemeana na aina ya tunda lenyewe. Ndani ya protini pia kuna tindikali (acid) aina ya amino.

VITAMINI "E": inadaiwa kuwa tunda hili lina kiwango kikubwa cha vitamini E kuliko ile inayopatikana kutoka kwenye mazao ya wanyama, hata mayai hayana kiwango kikubwa ukilinganisha na tunda la avocado.

VITAMINI "B6": Nayo inapatikana kwa wingi.

MADINI YA CHUMA (Iron): Pia yapo kwa wingi.


Baada ya kuvielezea baadhi ya virutubisho vinavyopatikana katika tunda hili, sasa tuangalie faida zinazotokana ama kwa kula au kutumia tunda la avocado au matumizi ya mmea wenyewe. Kwanza kabisa ningependa ujue kwamba majani ya mti wa avocado pamoja na magamba ya mti wake yakitengenezwa vizuri yanatumika kutibu maradhi ya kuharisha, kuondoa gesi tumboni, kutuliza kikohozi pamoja na matatizo ya ini na kusafisha njia ya mkojo. Dawa hii haishauriwi kutumiwa na akina mama wajawazito kwani inaweza kuwaletea matatizo yanayoweza kuharibu mimba. Aidha kwa wanawake ambao wameshindwa kuona siku zao kwa wakati, wanaweza kutumia mchanganyiko huo kwa nia njema ya kuwawezesha kuingia kwenye period.


Tunda la avocado ni chakula kizuri kwa watoto, pia lina madini ya potasiam (potassium) na vitamin B6 na E ambazo zinaweza kuleta nafuu kwa wale wenye matatizo ya stress, matatizo ya uzazi kama ugumba na uanithi. Tindikali aina ya oleic (oleic acid) iliyomo ndani ya tunda hili inasaidia kukinga dhidi ya magonjwa ya moyo, kiharusi na kansa. Aidha tunda hili linasaidia uyeyushaji wa chakula tumboni hasa kwa wale wenye matatizo ya vidonda vya tumbo, kwani tunda hili lina "fiber" ambayo ni muhimu kukinga kuta za utumbo. Watu wenye maradhi ya anaemia, diabetes, matatizo ya mfumo wa neva, matatizo ya artery wanashauriwa kula tunda hili mara kwa mara. Tunda la avocado limethibitishwa kupunguza kwa kiwango kikubwa cholesterol kutoka kwenye damu hasa kwa wale wenzangu na mimi ambao ni wanene.


Matumizi ya nje ya mwili kwa tunda hili husaidia kulainisha ngozi na kuondoa makwinyanzi, kung`arisha na kulainisha nywele na kuzifanya zionekane nadhifu, linasaidia ukuaji wa nywele na pia kuimarisha na kuzuia kukatika kwa nywele.


Hakika tunda hili lina maana sana kwa maisha yetu ya kila siku na inashauriwa kula tunda hili mara kwa mara kutegemeana na uwezo wako kwani hautopoteza chochote utakapokula tunda hili. Mada ijayo nitakupa vidokezo vichache namna ya kuandaa tunda hili kabla ya kuliwa.


Endelea kuwa pamoja nami katika toleo lijalo.


2FLAG.

Friday, August 22, 2008

TUNDA LA AVOCADO AU PARACHICHI


Natangulia kuwasalimu wapenzi wanablog. Bila shaka wote hamjambo. Leo ningependa niongelee juu ya tunda linaloonekana kwenye picha hapo juu. Tunda hili linajulikana kwa jina la Avocado, kwa lugha ya wenzetu, na kwa lugha yetu ya kiswahili tumezoea kuita kwa jina la Parachichi. Tunda hili lina majina mengi lakini nimeona niwatajie hayo mawili maana ndiyo "common" kwa watu walio wengi. Mimi binafsi, tunda hili nimelijulia hapa Bongo Darisalama nilipokuja miaka ile kwa mara ya kwanza. Siku ya kwanza kuonja tunda hili, sikulipenda na kwa kusema ule ukweli nililitema, maana sikuona ladha yeyote ile. Wakati huo, wale waliozoea kula tunda hili walinicheka sana.


Leo hii nawaambia, nimekuwa mlaji mzuri sana wa tunda hili, si kwamba ni tamu sana kuliko chochote, bali kutokana na umuhimu wake ambao nitauelezea hapo baadaye. Kwa asili, tunda hili limekuwa likizalishwa katika nchi zilizopo katika ukanda wa tropiki, hasa kule Amerika ya Kati. Lakini baadaye, zao hilo limesambaa na kulimwa maeneo mbalimbali hapa duniani. Huko nchi za ulaya wanalima, kule asia nako pia, hapa afrika napo tunajaribu na hata hapa Tanzania tumewekeza katika kilimo cha zao hilo muhimu kwa afya zetu. Maeneo machache yanayozalisha zao hili hapa nchini ni kama vile, kule kwa akina Mangi, yaani mkoani Kilimanjaro na kule kwa akina uswege, yaani mkoani Mbeya.


Kwa nini tunda hili lina umuhimu wa pekee! Labda ni kwa sababu ya virutubisho vyake vingi, vyenye uwezo wa kukinga na kutibu maradhi mbalimbali mwilini. Hebu fikiria kisa hiki;

" Hapo zamani za kale, palitokea mwanafunzi mmoja katika nchi za mbali, ambaye alifanya majaribio kwa kula avocado kwa kipindi cha mwezi mzima ikiwa kama ni mlo wake pekee kwa kila siku. Kijana huyo aliishi kwenye nyumba ya kupanga, na mwenye nyumba alichukua uamuzi wa kumfukuza katika nyumba yake, akihofia kuwa huenda angemletea matatizo na haibu endapo angemfia kwa kudhoofu kwa njaa. Lakini cha kushangaza kijana yule aliendeleza msimamo wake wa kula avocado kama alivyokusudia ingawa hakujua faida zinazopatikana kutokana na ulaji wa tunda hilo. Yule mwanafunzi alikuwa na ufahamu kidogo sana, kuwa matumizi ya muda mrefu ya tunda hilo yanaamsha ashki na kumfanya mtu awe na hamu na uwezo wa kutenda tendo la ndoa.
Hivi leo imethibitika kuwa tunda la avocado lina vitamini E ambayo ni muhimu katika kuimarisha mfumo wa uzazi kwa jinsia zote. Ukweli huu haupingani na ufahamu mdogo aliokuwanao yule kijana mwanafunzi wa enzi zile.

Tunda la avocado lina vitu gani zaidi ambavyo ni muhimu kwa afya yako, yangu na ya yule ndugu au jamaa yako! Endelea kufuatilia toleo lijalo. Tafadhali usikose, mwambie na mwenzio.
2FLAG

Thursday, August 21, 2008

KARIBUNI WAPENZI WANABLOG


Kwanza naomba nimshukuru Mungu kwa kunijalia na kunipa uzima, ambapo pia amenipa uwezo huu wa kujumuika na wanajamii wenzangu katika safu hii ya blog maridhawa itakayokuwa inakupa elimu juu ya mambo mbalimbali ya afya yako.


Ndugu msomaji wangu, nimependa tushirikiane katika jambo muhimu la kiafya ambalo kimsingi watu wengi wanaona tabu kutumia japo muda kidogo kusoma mambo yanayowahusu moja kwa moja, lakini watu hao wapo radhi kupoteza muda mwingi kusoma na kuangalia mambo yasiyowaletea manufaa.


Blog hii itakuwa inakupatia elimu, mwongozo, ushauri wa kutumia mazao ya chakula kama mbogamboga na matunda kwa kinga na tiba dhidi ya maradhi mbalimbali yanayoweza kuathiri afya ya mwili wako. Ninaposema kinga au tiba kwa kutumia mazao ya chakula au mimea haina maana kuwa ni tiba za uganga wa kienyeji, bali ni kinga au tiba mbadala kwani chakula unachokula kila siku ndicho kitatumika kama kinga au tiba kama utaweza kukipangilia vizuri.


Kwahiyo ninawakaribisha wote katika blog hii mchango wenu wa mawazo mazuri ndiyo utatufikisha mahali pazuri, kwani nitatoa fursa pia kuongelea masuala mengine ya kijamii.


KARIBUNI.


2FLAG