Tuesday, April 7, 2009

MWENDELEZO WA MADA YA AINA MBALIMBALI ZA JUISI



Habari za siku chache wadau wenzangu. Bila shaka baadhi yenu mnajiandaa na Sikukuu ya PASAKA kwani ipo jirani sana. Napenda niseme maandalizi mema.
Leo nitaendeleza kuwapatia aina nyingine za juisi na kazi zake mwilini. Kumbuka, juisi ninazozungumzia hapa ni zile za matunda halisi, kwa wale wanaojua lugha ya wenzetu wanasema "Fresh fruit juice". Hapa sizungumzii juisi za madukani ambazo zimefungwa kwenye maboksi au chupa na wakazibatiza kuwa ni za matunda halisi kumbe ni mchanganyiko wa madawa au kemikali zenye ladha ya matunda. Ningependa nikushauri kuwa ni vema ukatumia matunda yetu yatokayo kule Lushoto, Chanika, Rufiji, Moshi, Mbeya na kwingineko ili kutengenezea juisi na unufaike kiafya. Huo ni ushauri wa bure lakini maamuzi unayo mwenyewe.
Haya tuangalie aina za juisi zifuatazo:
  • JUISI YA MCHANGANYIKO WA NDIZI NA CHUNGWA: Chukua ndizi kama mbili au zinazotosha kutengenezea kiasi cha juisi upendacho na chungwa au machungwa. Kisha osha vizuri matunda yako na menya ndizi halafu zikate vipande vidogo. Ndizi ninazozungumzia hapa ni ndizi mbivu na si vinginevyo. Weka vipande vya ndizi zako kwenye blenda kisha saga upate juisi yako. Chukua chungwa au machungwa na kamua ili upate juisi yake kisha changanya na saga kwa pamoja ili upate mchanganyiko ulio sahihi. Chukua maji safi na salama kama glasi moja kisha changanya. Unaweza kuweka sukari au asali kidogo ili kuleta ladha. Unaweza kuweka mchanganyiko wa juisi yako kwenye friji ili ipate ubaridi kidogo na iwe tayari kwa matumizi.
  • FAIDA ZA JUISI HII KIAFYA: Kumbuka tunda la ndizi lina madini ya potasiam na sodiam kidogo. Madini haya yana vitamini B na pia kuna magneziam ndani yake. Virutubisho vilivyomo vinasaidia mzunguko wa damu kwenye arteri kuwa mzuri. Pia katika mchanganyiko huu wa juisi kuna vitamini C na A.
  • Aidha juisi hii inasaidia kutunza na kuufanya moyo ufanye kazi yake vizuri na ina uwezo wa kuzuia shinikizo la damu (High Blood Pressure).
  • JUISI YA MCHANGANYIKO WA APPLE NA PARACHICHI: Chukua maparachichi na apple zinazotosha kutengeneza kiasi cha juisi yako. Osha vizuri matunda yako kwa usalama wa afya yako kisha menya na ondoa mbegu. Kata vipande vinavyoweza kusagika. Weka kwenye sahani au bakuli kisha saga kwenye blenda ili upate mchanganyiko sahihi. Unaweza kuchanganya na asali vijiko vikubwa vya chakula viwili au vitatu na maziwa kidogo. Weka kwenye friji ipate ubaridi kidogo.
  • FAIDA ZAKE KIAFYA: Virutubisho vilivyomo ndani ya matunda haya vina uwezo mkubwa wa kupunguza cholesterol kwenye damu hivyo kupunguza uwezekano mkubwa wa mtumiaji wa juisi hii kupatwa na magonjwa ya arteri/kuziba kwa mishipa ya damu. Aidha mchanganyiko huu unazuia magonjwa kama anaemia (ukosefu wa madini ya chuma na upungufu wa damu mwilini), kwani parachichi na apple vina viwango vikubwa vya madini ya chuma. Pia huzuia kansa ya colon.

Kumbuka matumizi ya juisi hizi ni ya mara kwa mara. Unapokunywa juisi kama hizi mara moja kwa mwezi haitokusaidia kitu. Pangilia juisi hizi kama sehemu ya mlo wako wa kila siku.

Kwa leo naishia hapo tutaendelea siku zijazo.

NAWATAKIENI MAANDALIZI MEMA YA SIKUKUU YA PASAKA NA PASAKA NJEMA.





1 comment:

Anonymous said...

Asante mzee wa uelimishaji juu ya lishe mbadala kwa afya zetu. Mimi binafsi nina tatizo la kukosa hamu ya kula na matokeo yake nakula chakula kidogo sana kiasi kwamba hata mke wangu nyumbani anakosa imani na mimi akidhani kuwa ninakula kwingineko kwani tatizo hili halikuwapo hapo awali. Naomba ushauri wako ili nipate ufumbuzi wa tatizo hili. Ukweli sina maumivu mahali popote.
Asante.