Wednesday, August 27, 2008

JE, NITAKULA NINI AU UTAKULA NINI NA KWA KIASI GANI?


Habari za mihangaiko wadau wenzangu! Hongereni kwa kazi. Nasema hongera kwa kazi na siyo pole kwa kazi kwani viongozi wetu wametuhasa tuseme hongera badala ya pole. Maana pole anapewa mtu mwenye matatizo. Nasema hivyo kwa sababu kazi siyo matatizo ila ukikosa kazi ndipo matatizo mengi hujitokeza.


Nawashukuru wadau wenzangu kwani nimepokea baadhi ya maoni na maswali kutoka kwa wasomaji wakitaka kujua watumie chakula gani, kwa kiwango ama kiasi gani, katika muda gani, na kwa wale ambao walishakula sana vyakula nilivyovitaja katika mada yangu iliyotangulia juu ya dokezo la EAT AT YOUR OWN RISK, wafanye nini ili kuepuka kupatwa maradhi yanayosababishwa na ulaji wa vyakula hivyo.


Jibu rahisi ambalo naweza kukupatia kwa haraka nitakuambia kula kulingana na mahitaji ya mwili wako. Lakini, je, utajuaje mahitaji ya mwili wako? Mdau mwenzangu nitakuomba tuendelee kuwa pamoja maana zipo mada maalum zitakazojibu maswali hayo yote kwa ufasaha. Hata kama umekula sana vyakula hivyo na ukajihisi kuwa ni mnene, blog hii itakupatia fomula mbalimbali ambazo unaweza kuzitumia kupunguza unene.


Kwa ufupi rejea kwenye hilo jedwali hapo juu la mpangilio wa vyakula. Kwa wale wasomi wa lugha ya wenzetu wanaliita "A Pyramid of Balanced Diet". Jedwali hilo linakupa namna ambavyo unaweza kupangilia mlo wako wa kila siku, na kula chakula unachopaswa kula kwa kiasi na kiwango unachotaka kwa afya yako. Kwa mfano ukianzia chini ambako nafasi ni pana inamaanisha unatakiwa ule kwa wingi vyakula hivyo na kwa kadri unavyopanda juu unashauriwa upunguze kula chakula kilichoelezwa katika makundi hayo ya vyakula.



  1. Unashauriwa ule kwa wingi vyakula vya nafaka kama wali, ugali, mkate n.k, ingawa hapa watu wengine hawataki kabisa kusikia habari za ugali labda wale watu waliokulia bara.


  2. Kula kwa wingi vyakula vya mbogamboga na matunda maana yakula hivi vina virutubisho vyote na ni kinga na dawa kwa baadhi ya maradhi mwilini .


  3. Kula kwa kiasi kidogo vyakula vyenye protini nyingi hasa vile vinavyotokana na mazao ya wanyama kama vile; nyama, kuku, mayai, maziwa, mtindi, samaki na maharage makavu n.k, ukiweza kula vyakula vya aina hii mara moja kwa wiki.


  4. Ukiweza, acha kabisa ama kula kidogo sana vyakula vyenye asili ya mafuta ama vilivyoongezwa mafuta, vilivyoongezwa sukari. Najua wengi wanapenda kula vyakula vilivyokaangizwa, ukiwaambia wapike ama wale chukuchuku wanakujibu kwani nina shida gani, raha jipe mwenyewe, kumbe hawajui ndiyo kwanza wanatengeneza shida zitakazowapa karaha badala ya raha.

Najua ni vigumu kwa watu kufuata mpangilio huu. Lakini kama umedhamiria kuilinda afya yako unaweza na tena vyakula hivyo ni rahisi kuvipata katika masoko yetu hapa nchini TZ tofauti na wenzetu kule majuu.


Aidha niliposema kula kulingana na mahitaji ya mwili wako, unapaswa kujua wewe mwenyewe unafanya shughuli gani. Kwasababu, mahitaji ya miili yanatofautiana kulingana na aina ya shughuli au kazi ya mtu husika. Kwa mfano watu wanaofanya kazi maofisini na walimu wanahitaji kiasi kidogo cha chakula; kwa wanafunzi na wafanyabiashara na wachuuzi pamoja na watumishi wa kazi za ndani wanahitaji nyongeza kidogo tofauti na mtu wa ofisini; mafundi kama seremala, umeme, watumishi wa nyumbani wanaofanya kazi kama za kulisha mifugo na nyingine ngumu wanahitaji chakula cha kutosha; na wafanyakazi wa ujenzi kama wabeba zege, ujenzi wa barabara, migodini, wanariadha na wengine wa aina hiyo wanahitaji chakula kingi ili kutosheleza mahitaji ya miili yao kwani wao wanatumia calories nyingi. Hivyo ni vema ukazingatia hilo ili usije kula chakula zaidi ya mahitaji ya mwili wako na matokeo yake ni unene unaoweza kukusababishia matatizo au hata usipokuwa mnene unaweza kujikuta unapata kisukari kinyume na matarajio yako.


Kwa maelezo hayo nadhani nitakuwa nimejibu baadhi ya maswali ya wasomaji waliotaka kujua watakula nini, kwa kiasi na kiwango gani na wakati gani. Kumbuka, hapo baadaye nitakupa jinsi unavyotakiwa kupangilia milo yako kwa siku. Kama una maswali zaidi usisite kuuliza.


Asante kwa ushirikiano wenu na karibu tena.





2 comments:

Anonymous said...

Sawa mdau, mimi binafsi ni mwili wangu ni mnene, ninatamani niwe na mwili wa kawaida. Nimejaribu njia mbalimbali za kushinda na njaa kwa kula mlo mmoja kwa siku lakini unene uko pale pale. Nimejaribu kunywa maji ya moto kila siku asubuhi lakini hali bado ni ileile. Naomba unishauri ndugu yangu nifanyeje? Asante kwa msaada wako.

Anonymous said...

Jamani mie ni mnene kiasi ambao ni wa kawaida tu na wengi wanao..ila nina kitambi sijui kimetoka wapi..sipendi.nimekuwa nikifanya mazoezi na kuacha kula wakati mwingine japo nakuwa weak sana ila kitambi bado kipo..nakuwa nipo fiti na afya lakini kitambi kimeniganda..sinywi pombe kabisa..sasa nifanyeje ..je ni vyakula????naomba njia rahisi na ya muda mfupi na natural ..