Monday, August 25, 2008

UNAFAHAMU NAMNA UNAVYOWEZA KULA TUNDA LA AVOCADO

Kimsingi avocado au parachichi siyo tunda kama tunavyofikiria bali ni jamii ya mbogamboga. Hii inatokana na ukweli kwamba tunda hilo limekosa baadhi ya vitu vinavyoleta utamu ambavyo vinapatikana kwenye matunda mengine tuliyoyazowea hivyo avocado limekosa sifa ya kuwa katika jamii ya matunda isipokuwa lipo katika jamii ya mbogamboga. Tunda hili linaweza kuandaliwa na kuliwa katika namna tofauti kama ifuatavyo:

  • fruit salad, yaani mchanganyiko wa matunda mbalimbali yaliyoandaliwa kwa kukatwakatwa vipande vidogo na kukamuliwa limao kwa ajili ya kuongeza ladha. Maandalizi ya mchanganyiko huu ni rahisi kwani muandaaji anatakiwa kuchukua avocado na matunda mengine kama vile ndizi, matango, mapapai, zabibu n.k na kisha kuyaosha na kuyamenya ambapo mchanganyiko huo unaweza kuhifadhiwa kwenye jokofu ili upate ubaridi kidogo kabla ya kuliwa. mchanganyiko huu pia unaweza kuongezwa maziwa kama utapenda

  • Vegetable salad, huu ni mchanganyiko wa avocado na jamii ya mbogamboga zilizoandaliwa kwa kukatwakatwa vipande. Mchanganyiko huu unaweza kuhusisha mboga kama nyanya, cabbage, pilipili hoho, n.k. Pia katika mchanganyiko kama huu unaweza kuweka limao ili kuleta ladha fulani mdomoni. Kwa wenzetu hupenda kuweka aina fulani ya mafuta kama vile olive oil ili kuipa ladha zaidi. Lakini kama uwezo wetu hauruhusu mambo hayo basi siyo lazima sana kwani vitu vya msingi utakuwa umevipata. Maandalizi yake hayana tofauti na yale ya fruit salad.

  • Juisi, tunda la avocado ni zuri kwa kutengenezea juisi. Inashauriwa upate avocado lililoiva vizuri ili iwe rahisi kulisaga. Unaweza kutengeneza juisi ya avocado pekee au unaweza kuchanganya na tunda jingine kama vile apple, pensheni, embe n.k. Utengenezaji wa juisi unategemea uwepo wa vifaa kama juicer au blenda. Lakini kama hauna uwezo wa kupata au kununua vitu hivyo ambavyo pia vinatumia umeme, unaweza kutumia kinu kidogo kusaga ili kupata mchanganyiko uliosagika vizuri kisha kupata juisi uliyoikusudia. Wakati mwingine inabidi tukumbuke tulikotoka ambapo wazee wetu walikuwa wanatengeneza dawa za aina hiyo kwa kutumia vifaa hivyo vya asili.

  • Fresh fruit, unaweza kula avocado kama lilivyo kwa kulimenya na kuondoa mbegu yake. Lakini zingatia usafi kabla ya kula tunda hilo usije ukapatwa na maradhi ya tumbo.

  • Avocado linaweza kutengenezwa cream na ikaliwa kama ile uliyozowea kununua kwenye maduka ya Bakhresa. Hii inahitaji hatua fulani ili uweze kupata kitu ulichokikusudia.

  • Avocado linaweza kupakwa kwenye mkate mfano wa siagi. Kama utapenda unaweza kutumia chumvi kidogo ili kuongeza ladha.

Kumbukeni unapoandaa vitu hivyo hapo juu ni lazima uzingatie usafi ukianzia wewe mwenyewe, vyombo utakavyotumia pamoja na matunda, siyo lazima upate matunda yote ili kukamilisha mchanganyiko ulioelezewa hapo juu, bali unaweza kuchukua baadhi kutegemeana na uwezo wako ili mradi tunda la msingi kama avocado lipo kwenye mchanganyiko wako. Matunda haya yapo karibu kila kona za mitaa ya Darisalama kwa wale waliopo jiji hilo, pia yanapatikana baadhi ya mikoa hapa nchini, hivyo siyo mpaka ushauriwe na daktari ndipo ule matunda, anza sasa kula matunda, japo moja kwa siku si haba.

Kwa wale watakaohitaji kujua maandalizi na matumizi ya avocado kwa ajili ya kutunza nywele au ngozi wanaweza kuwasiliana nami kupitia email zifuatazo: larkado@gmail.com au leofiderk@yahoo.com

Asante.

2FLAG









2 comments:

Anonymous said...

nashauri pia mtufundishe jinsi ya kupika vyakula na vitafunwa,Mi natamani kujua jinsi ya kupika sambusa na katless.

hajra said...

Pongezi nyingi kwako kwa kuendeleza blog hii Mungu akuwezeshe zaidi.

Naomba tuelekezwe jinsi ya kutengeneza keki za aina mbalimbali pamoja na Icing sugar.

Ahsante.