Friday, August 29, 2008

IJUE KAROTI NA FAIDA ZAKE

Habari za maisha wadau wenzangu! Naomba leo niwape japo kidogo kuhusu matumizi ya zao la karoti pamoja na faida zinazopatikana kutokana na utumiaji wa zao hilo, ambalo kimsingi mizizi yake ndiyo hasa zao lenyewe. Napenda niwaombe radhi wale ndugu zangu waliouliza maswali juu ya kujikinga ama namna ya kuondokana na unene. Mada inayohusu unene na athari zake nitaitoa wiki ijayo na nitakupa dokezo ambazo zitakusaidia kuondokana na unene au kitambi.

Tukirudi kwenye mada ya leo, kumbuka kuwa karoti inalimwa karibu kila pembe ya dunia hii. Zao hili linatofautiana katika rangi, kwani kuna karoti nyeusi, zenye rangi ya pinki, nyekundu na njano. Karoti yenye rangi nyekundu na njano ndiyo hasa tunayolima hapa TZ. Karoti za rangi nyekundu na njano ndizo zinasemekana kuwa na virutubisho vingi sana kuliko karoti nyingine.

Karoti ina protini kidogo na haina mafuta kama tulivyoona kwa tunda la avocado. Pia ina asili ya wanga, na ni chanzo kizuri cha vitamini B, C na E. Aidha ina madini mengi ikiwemo madini ya chuma. Kuna kitu kinaitwa beta-carotene ambayo imo ndani ya karoti na hii ikiingia mwilini inabadilishwa na kuwa vitamini A. Vile vile karoti ina kirutubisho kinachoitwa fiber ambacho ni muhimu kwa kukinga kuta za utumbo.
Karoti ikitumiwa vizuri na tena mara kwa mara inasaidia kukinga na kuponya magonjwa yafuatayo: macho hasa kutoona gizani au kwenye mwanga hafifu, ngozi, kupunguza tindikali inayodhuru tumboni na kukinga magonjwa yenye asili ya kansa.


Karoti inaweza kuliwa kwa namna mbalimbali kama vile, ikiwa mbichi kwa kutafuna, inaweza kupikwa na kuchanganywa na mbogamboga zingine, inaweza kusagwa na kupata juisi ambayo pia inaweza kuchanganywa na juisi zingine, aidha kukatwakatwa na kuchanganywa kwenye salad ya matunda au mbogamboga. Machicha ya karoti iliyosagwa yanaweza kutumika kama dawa kukinga ama kuponya maradhi ya nje ya mwili.
Mada nyingine nitazungumzuzia kazi ya virutubisho vilivyomo ndani ya karoti.

KILA LA HERI NA TUONANE SIKU NYINGINE MUNGU AKIPENDA.

No comments: